Sauti ya Mtu aliaye
Nyikani.!
Luka 3: 3 - 5, Isaya 40: 3 – 6
Mpendwa msomaji naomba tutafakari Neno la Mungu kwa
kuangalia kwa undani Ujumbe wa Yohana Mbatizaji ambaye Biblia humwita
mtangulizi wa Yesu. Sauti ya mtu aliaye nyikani ni maneno ambayo tunayaona
yamesemwa na nabii Isaya zamani za kale lakini yanaonekana Dhahiri wakati
ambapo Yohana Mbatizaji anaanza kuhubiri. Maneno haya ” Sauti ya Mtu aliaye Nyikani” ni maneno yanayoashiria ujumbe wa
huzuni kwamba kuna mtu anatoa sauti mahali ambapo hakuna watu ambao
wanamsikiliza.
Yohana anaonekana kuwa ndiye mtu huyo na nyika ni dunia
ambayo imejaa watu lakini hakuna anayesikiliza anachosema Yohana. Sasa ukisoma
maneno haya utagundua kuwa huu ni ujumbe wa siku za mwisho wenye maonyo ili
kuwatayarisha watu kuwa kuna jambo linakuja. Kama ilivyokuwa kipindi cha Nuhu
watu walimwona Mzee Nuhu kama amechanganyikiwa hata alipomaliza safina
hawakuweza kuingia.
Yohana ni Nani? Luka
5 - 25.
Yohana Mbatizaji ni mtoto wa Zakaria na Elizabeth hawa ni
wazazi ambao Biblia inasema kuwa walikuwa ni wenye Haki wasio na lawama mbele za Mungu na wanadamu. Walikuwa wakimcha
Mungu na Zakaria alikuwa ni Kuhani. Pia wazazi hawa walikuwa ni wazee sana hata
matumaini ya kupata mtoto yalikuwa hakuna tena kwani Elizabeti alikuwa tasa.
Pamoja na changamoto aliyokuwa nayo Zakaria lakini bado alikuwa
akimcha na kumtumikia Mungu. Hapa tunaona Zakaria anakutana na Malaika ndani ya
hekalu. Ni katika nyumba ya Mungu pekee
ndipo unaweza kupata ujumbe wa Mungu. Watu wengi hukata tamaa mara wanapoona
mambo yao hayaendi vizuri na kuona kwamba labda Mungu amewaacha, jambo
linalowafanya wengine kuacha kabisa hata kwenda kanisani. Kumbuka Kanisani ndio
mahali pekee ambapo unaweza kusikia ujumbe wa Mungu ambao unaweza kubadili
maisha yako.
Wakati Zakaria akitekeleza
majukumu yake ya ukuhani Malaika Gabriel alimtokea na kumpa ujumbe wa faraja na
furaha kuwa Elizabeti atazaa mtoto na jina lake atamwita Yohana. Ukiangalia
tukio la kuzaliwa kwa Yohana halina tofauti sana na tukio la kuzaliwa kwa Yesu.
- Wote wanazaliwa katika Familia ya wazazi wenye Haki (Luka 1: 6 na Math 1: 19).
- Ujumbe wa kuzaliwa kwao uliletwa na Malaika mmoja Gabriel. (Luka 1:19 na Luka 1:26).
- Majina yao yametajwa na Malaika (Luka 1:13 na Luka 1: 31).
Yohana anakuja na ujumbe wa kuwaandaa watu kwa ajili ya
masihi anayekuja ambaye yeye mwenyewe anasema hawezi hata kulegeza gidamu ya
viatu vyake.
Ujumbe wa Yohana. Luka
3: 7 – 14.
Yohana alihubiri ujumbe wa toba ili kuwaandaa watu kumpokea
Kristo ambaye anakuja. Swali langu kwa nini alihubiri toba liletalo ondoleo la
dhambi. Mpendwe msomaji huwezi kumkaribia Mungu kama uu mwenye dhambi ila tuna
ujasiri wa kumkaribia Mungu kwa toba na rehema. Kama moyo wa si safi ni kazi
sana kumkaribia Mungu ili akuokoe. Toba ya kweli huleta ondoleo la dhambi, Toba
hufungua mlango kwa Mungu kukusaidia na kukulinda. Toba hufungua mlango wa
maombi yako kujibiwa. Maana Mungu ni Mtakatifu na amesema iweni watakatifu kama
mimi nilivyo mtakatifu. IPetro 1: 15 – 16.
Dhambi zetu hututenga na Mungu Isaya 59: 1 – 2. Hivyo kama
unahitaji kurejesha uhusiano wako na Mungu lazima utubu ili mausiano yako na
Mungu yarudi. Yohana aliwaandaa watu kutubu ili kujiandaa kumpokea Yesu, vivyo
hivyo hata sisi leo tunatazamia tumaini kuu la mataifa yote la kurudi kwa Yesu
hatuwezi kumsubiri Yesu arudi wakati tuko katika maisha ya dhambi. Ni wajibu wa
kila mmoja wetu kujitafakari na kutubu ili Yesu akija akukute uko tayari. Maana
Yohana anasema yeye atawabatiza kwa Roho na kwa moto. Kumbuka unapokusana na
Muumba wako ni kama umekosana na kila kitu alichokifanya kwa ajili yako, ndio
maana maisha yako yamekuwa si mazuri kwa sababu mahusiano yako na Mungu ni
mabaya. Fungua moyo wako mkaribishe Yesu kwa toba ya kweli !!
Neno litaendelea!!
Kwa maneno haya mafupi kama umeamua kwa moyo wako wote
kumrudia Mungu.
Kiri sala hii ya toba
kwa Imani nawe utaokoka!!
‘Eeh Yesu nimejua makosa yangu na nimegundua kuwa nimekuwa mbali na uso
wako kwa dhambi nilizozifanya. Naomba unirehemu sawasawa na fadhili zako,
Uyafute makosa yangu, unioshe na uovu wangu, Unitakase dhambi zangu, na uandike
jina langu kwenye kitabu cha Uzima.
Eeh Mungu uniumbie moyo safi, usinitenge na uso wako, unipe nguvu za
kushinda dhambi, unijaze na Roho wako Mtakatibu. Karibu Yesu moyoni mwangu.
Kuanzia leo nimeokoka !! Ameen!!’