Luka 3: 3 - 5, Isaya 40: 3 – 6
Mpendwa msomaji naomba tutafakari Neno la Mungu kwa kuangalia kwa undani Ujumbe wa Yohana Mbatizaji ambaye Biblia humwita mtangulizi wa Yesu. Sauti ya mtu aliaye nyikani ni maneno ambayo tunayaona yamesemwa na nabii Isaya zamani za kale lakini yanaonekana Dhahiri wakati ambapo Yohana Mbatizaji anaanza kuhubiri. Maneno haya ” Sauti ya Mtu aliaye Nyikani” ni maneno yanayoashiria ujumbe wa huzuni kwamba kuna mtu anatoa sauti mahali ambapo hakuna watu ambao wanamsikiliza.
Yohana anaonekana kuwa ndiye mtu huyo na nyika ni dunia ambayo imejaa watu lakini hakuna anayesikiliza anachosema Yohana. Sasa ukisoma maneno haya utagundua kuwa huu ni ujumbe wa siku za mwisho wenye maonyo ili kuwatayarisha watu kuwa kuna jambo linakuja. Kama ilivyokuwa kipindi cha Nuhu watu walimwona Mzee Nuhu kama amechanganyikiwa hata alipomaliza safina hawakuweza kuingia.
Yohana ni Nani? Luka 5 - 25.
Yohana Mbatizaji ni mtoto wa Zakaria na Elizabeth hawa ni wazazi ambao Biblia inasema kuwa walikuwa ni wenye Haki wasio na lawama mbele za Mungu na wanadamu. Walikuwa wakimcha Mungu na Zakaria alikuwa ni Kuhani. Pia wazazi hawa walikuwa ni wazee sana hata matumaini ya kupata mtoto yalikuwa hakuna tena kwani Elizabeti alikuwa tasa.
Pamoja na changamoto aliyokuwa nayo Zakaria lakini bado alikuwa akimcha na kumtumikia Mungu. Hapa tunaona Zakaria anakutana na Malaika ndani ya hekalu. Ni katika nyumba ya Mungu pekee ndipo unaweza kupata ujumbe wa Mungu. Watu wengi hukata tamaa mara wanapoona mambo yao hayaendi vizuri na kuona kwamba labda Mungu amewaacha, jambo linalowafanya wengine kuacha kabisa hata kwenda kanisani. Kumbuka Kanisani ndio mahali pekee ambapo unaweza kusikia ujumbe wa Mungu ambao unaweza kubadili maisha yako.
Wakati Zakaria akitekeleza majukumu yake ya ukuhani Malaika Gabriel alimtokea na kumpa ujumbe wa faraja na furaha kuwa Elizabeti atazaa mtoto na jina lake atamwita Yohana. Ukiangalia tukio la kuzaliwa kwa Yohana halina tofauti sana na tukio la kuzaliwa kwa Yesu.
- Wote wanazaliwa katika Familia ya wazazi wenye Haki (Luka 1: 6 na Math 1: 19).
- Ujumbe wa kuzaliwa kwao uliletwa na Malaika mmoja Gabriel. (Luka 1:19 na Luka 1:26).
- Majina yao yametajwa na Malaika (Luka 1:13 na Luka 1: 31).
Yohana anakuja na ujumbe wa kuwaandaa watu kwa ajili ya masihi anayekuja ambaye yeye mwenyewe anasema hawezi hata kulegeza gidamu ya viatu vyake.
Ujumbe wa Yohana. Luka 3: 7 – 14.
Yohana alihubiri ujumbe wa toba ili kuwaandaa watu kumpokea Kristo ambaye anakuja. Swali langu kwa nini alihubiri toba liletalo ondoleo la dhambi. Mpendwe msomaji huwezi kumkaribia Mungu kama uu mwenye dhambi ila tuna ujasiri wa kumkaribia Mungu kwa toba na rehema. Kama moyo wa si safi ni kazi sana kumkaribia Mungu ili akuokoe. Toba ya kweli huleta ondoleo la dhambi, Toba hufungua mlango kwa Mungu kukusaidia na kukulinda. Toba hufungua mlango wa maombi yako kujibiwa. Maana Mungu ni Mtakatifu na amesema iweni watakatifu kama mimi nilivyo mtakatifu. IPetro 1: 15 – 16.
Dhambi zetu hututenga na Mungu Isaya 59: 1 – 2. Hivyo kama unahitaji kurejesha uhusiano wako na Mungu lazima utubu ili mausiano yako na Mungu yarudi. Yohana aliwaandaa watu kutubu ili kujiandaa kumpokea Yesu, vivyo hivyo hata sisi leo tunatazamia tumaini kuu la mataifa yote la kurudi kwa Yesu hatuwezi kumsubiri Yesu arudi wakati tuko katika maisha ya dhambi. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kujitafakari na kutubu ili Yesu akija akukute uko tayari. Maana Yohana anasema yeye atawabatiza kwa Roho na kwa moto. Kumbuka unapokosana na Muumba wako ni kama umekosana na kila kitu alichokifanya kwa ajili yako, ndio maana maisha yako yamekuwa si mazuri kwa sababu mahusiano yako na Mungu ni mabaya. Fungua moyo wako mkaribishe Yesu kwa toba ya kweli !!
Neno litaendelea!!
Kwa maneno haya mafupi kama umeamua kwa moyo wako wote kumrudia Mungu.
Kiri sala hii ya toba kwa Imani nawe utaokoka!!
‘Eeh Yesu nimejua makosa yangu na nimegundua kuwa nimekuwa mbali na uso wako kwa dhambi nilizozifanya. Naomba unirehemu sawasawa na fadhili zako, Uyafute makosa yangu, unioshe na uovu wangu, Unitakase dhambi zangu, na uandike jina langu kwenye kitabu cha Uzima.
Eeh Mungu uniumbie moyo safi, usinitenge na uso wako, unipe nguvu za kushinda dhambi, unijaze na Roho wako Mtakatibu. Karibu Yesu moyoni mwangu. Kuanzia leo nimeokoka !! Ameen!!’
No comments:
Post a Comment